Nyakati za mwisho
SOMO: MWISHO WA DUNIA HII UMEKARIBIA
Mwl: Fredrick Kapaya
E-mail: kapayafarajaph@gmail.com
2 Timotheo 3:1
"Lakini ufahamu neno hili,ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari"
Lengo la somo: Ni kukukumbusha ya kuwa tupo kwenye nyakati za mwisho kwa sababu hiyo kila mtu anahitaji kuwa na maandalizi mazuri ili awe na nafasi katika uzima wa milele.
Mambo ya msingi
- Elewa ya kuwa kila jambo lina mwanzo wake na mwisho wake, mwanzo wa hii dunia ulikuwepo kwa sababu hiyo elewa kuwa mwisho wa dunia hii utakuwepo
- Upo uwezekano wa kuanza jambo fulani vizuri halafu ukamaliza vibaya, kumaliza vizuri au vibaya hutegemea sana ulichokuwa unakifanya kabla haujafika mwisho. Mwisho mbaya hufuta yote mazuri uliyoyafanya kisha tabia yako inaanza kuelezeka kwenye mwisho wako na sio kwenye mwanzo wako.
- Fanya yote hapa duniani kwa kadri unavyoweza ila kumbuka kuwa kila jambo lina mwisho wake.
Chochote unachokifanya hapa duniani kizuri au kibaya kinatengeneza aina fulani ya maisha yako ya badae lakini pia kufanya jambo fulani kwa juhudi au kwa ulegevu unaweza ukawa ni uamuzi wa mtu husika kwa kadri anavyoona umuhimu wa hilo jambo analolifanya.
Mathayo 6:33
"Bali utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa"
Biblia inaposema tuutafute kwanza ufalme wa Mungu inaonesha umuhimu wa ufalme wa Mungu ndani ya maisha ya mtu katika ulimwengu huu na ujao, haya mengine tunayofanya ni nyongeza.
Watu wengi sana wameonekana kujibidiisha sana katika kutengeneza maisha yao ya sasa na ya baadae ambayo ni ya kupita tu (si jambo baya kuwa na maisha mazuri), lakini wengi pia wamesahau kuwa wanatakiwa kuutumia muda wao mwingi zaidi kutengeneza maisha yao katika ulimwengu ujao ambayo ni ya milele.
Yakobo 4:14
"Walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka"
Lakini pia unaweza ukawa na maisha mazuri sana hapa duniani kiasi ambacho ukaishi kwa raha sana na kuwadharau wengine ambao ni maskini, umesahau ya kuwa wewe ni wa kupita tu na hayo unayofanya yatapita tu.
Luka 16:19- 24
"Akasema, palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa. Na maskini mmoja jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri, hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake, akalia akisema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu"
Kumbuka kuwa:
- Yeyote anayetafuta kutoshelezwa kwa nafsi yake (kwa anasa za dunia hii) atapoteza kutoshelezwa katika ulimwengu ujao.
- Mwanadamu anayeipenda dunia hii na kuishi pasipo kumtii Mungu, mwisho wake katika dunia hii ndio utakuwa mwanzo wake wa mateso ya milele maana biblia inasema baada ya kifo ni hukumu.
Waebrania 9:27
"Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa ni hukumu"
- Ila yule anayeteseka na kudharauliwa na watu maadamu ndani yake amempokea Yesu kisha anaishi maisha ya ushuduhuda mwisho wake katika dunia hii ndio utakuwa mwanzo wake wa kupata burudiko la milele.
- Bado unao wakati wa kutengeneza uwapo hai, nasema nawe mpendwa tengeneza maisha yako haujui kesho yako lakini pia karibu Yesu anakuja kulichukua kanisa lake.
Tupo katika siku za mwisho, zipo dalili zinazoonesha ya kwamba hizi ni nyakati za mwisho, lekebisha maisha yako mpendwa, usijisahau, usimwabudu Mungu kwa mazoea, usifanye kazi ya Mungu kwa mazoea. Oh!
Hizi ndizo dalili zinazoonesha kuwa tuko katika nyakati za mwisho
- Watu wamekuwa wakijipenda wao wenyewe, upendo wa ndugu umepoa kabisa cha kushangaza zaidi hata baadhi ya wapendwa wamepoteza upendo wa kweli wamebaki na tabia ya unafiki, wanawasema wengine vibaya, wanawachukia wakristo wenzao.
2 Timotheo 3:1-6
"lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiopenda wa kwao, wasio taka suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake"
- Maarifa yameongezeka kwa kasi, maarifa haya yamewasaidia watu wengine kufanya yaliyomema lakini wengine wameyatumia katika kufanya mambo mabaya sana ambayo ni chukizo mbele za Mungu.
Danieli 12:4
"Lakini wewe, Ee Daniel, yafunge maneno haya, ukakitie muhuri kitabu, hata wakati wa mwisho: wengi wataenda mbio huko na huko, na maarifa yataongezeka"
- Matukio mbalimbali mabaya yanatokea vita, njaa zinatokea, matetemeko yanatokea haya yote yanaonesha ya kuwa tuko nyakati za mwisho.
Mathayo 24:7
"Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali. Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu"
Mungu akubariki sana
Comments
Post a Comment